Mwanamuziki nguli wa RnB kutoka Marekani, R. Kelly, ameripotiwa kukimbizwa hospitalini baada ya kupoteza fahamu akiwa ndani ya chumba chake cha gerezani la ‘Butner Federal Correctional Complex’, lililopo North Carolina.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 58 alizimia ghafra baada ya kupewa kiasi cha dawa ambacho kinaelezwa kuwa huwenda kingehatarisha maisha yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ‘AllHipHop’, Kelly alipewa dawa hizo na wahudumu wa afya wa gereza, lakini wingi wake umeibua maswali mengi kuhusu uangalizi wa afya ya mfungwa huyo anayekabiliwa na kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono na mengineyo.
Mawakili wake wameeleza kuwa hali ya msanii huyo ilibadilika ghafla baada ya kutumia dawa hizo, na kusababisha kuanguka chumbani kwake bila msaada wa haraka. Baada ya kushindwa kupata fahamu ndani ya muda mfupi, uongozi wa gereza uliamua kumkimbiza hospitalini ili kupatiwa matibabu zaidi.
Hii siyo mara ya kwanza kwa afya ya R. Kelly kuibua wasiwasi gerezani. Tangu aanze kutumikia kifungo chake, amekuwa akisumbuliwa na magonjwa kama shinikizo la damu na kisukari, hali inayomlazimu kutumia dawa mara kwa mara. Kwa sasa, ripoti zinaeleza kuwa hali yake imeanza kuimarika baada ya kupata matibabu hospitalini.
Aidha tatizo hili linakuja zikiwa zimepita siku tano tuu tangu timu ya wanasheria wa Kelly kuomba msanii huyo aachiliwe mara moja kutoka gerezani na apewe kifungo cha nyumbani, hii ni baada ya maisha yake kuwa hatarini katika gereza hilo.
Mawakili hao walidai kuwa kunaushahidi wa wazi unaowalenga maafisa wa polisi kupanga njama ya kumuua Kelly katika gereza la Serikali huko North Carolina, ambapo anatumikia kifungo chake cha miaka 30.
Katika ushahidi wao, waliwasilisha tamko la kiapo kutoka kwa Mikeal Glenn Stine, mfungwa anayetumikia kifungo cha maisha (terminally ill), ambaye alidai kuwa maafisa wa gereza walimshawishi amuue Kelly kwa ahadi ya kuachiwa huru.
R. Kelly, ambaye jina lake kamili ni Robert Sylvester Kelly, amehukumiwa miaka 30 jela kufuatia makosa mbalimbali yanayohusisha unyanyasaji wa kingono, usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono (sex trafficking) na uongo kwa mamlaka.
Hukumu hiyo ilitolewa mwaka 2022 baada ya kupatikana na hatia kwa kutumia umaarufu wake kuwadhulumu kingono wanawake na wasichana wadogo kwa kipindi cha miaka mingi.

Leave a Reply