Diamond alivyobadilisha biashara ya Jux hadi kimataifa

Diamond alivyobadilisha biashara ya Jux hadi kimataifa

Peter Akaro

Tayari mastaa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Jux wapo Uingereza kwa ajili ya show tatu zitakazofanyika London, Manchester na Glasgow hadi Juni 15, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wawili hawa kutumbuiza pamoja nje ya Afrika.

Kwa Diamond ni jambo alilozoea kwa miaka mingi ila kwa Jux ni hatua kubwa kwake kwa sasa anapolitafuta soko la kimataifa kufuatia staa huyo wa WCB Wasafi kuchangia kubadilisha biashara yake tangu kolabo yao ya pili.

Awali Jux alikuwa anafanya muziki wa RnB na ndio ulimtambulisha kwa wengi, akiwa na miaka zaidi ya 10 katika muziki na chati yake kimuziki ikianza kushuka, aliamua kubadilika ili kuendelea kuwepo masikioni mwa mashabiki.

Ndipo akageukia miondoko ya Amapiano na Afro Pop, huku akutana na S2kizzy, Mtayarishaji Muziki na Mkurugenzi wa studio za Pluto Republic, pamoja na Diamond ambaye ni Mkurugenzi wa WCB Wasafi, lebo iliyowatoa mastaa kibao.

Tayari Diamond amesikika katika nyimbo tatu za Jux, Sugua (2019), Enjoy (2023) na Ololufe Mi (2024), zote zikitayarishwa na S2kizzy ambaye umaarufu wake ulikuja baada ya kutengeneza ngoma ya Country Wizzy, Aah Wapi (2016).

Oktoba 2024, video wimbo ‘Enjoy’ iliyotayarishwa na Director Fole X na kuachiwa Oktoba 7, 2023, iliweka rekodi ya kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikiwa ni video ya kwanza ya Bongo Fleva kufanya hivyo ndani ya muda mfupi zaidi.

Hii pia ni video ya kwanza kwa Jux kufikia namba hizo ila ndani ya Bongo ilikuwa ni ya nane huku Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, akiwa msanii wa nne kwa ujumla kufanya hivyo.

Ikumbukwe hadi sasa Diamond ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, anazo tano ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020 na Nana (2015).

Na wote wanaomfuatia Diamond wana video moja moja, video ya Harmonize iliyofanya hivyo ni Kwangwaru (2018), Zuchu ni Sukari (2021), Jux ni Enjoy (2023) na Rayvanny ni Number One (2020).

Wimbo huo (Enjoy) ulishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2023, lakini Jux alidai kuwa wimbo huo ulipaswa kuwania vingi zaidi na sio hicho kimoja tu ambacho ulipewa nafasi.

Kwa mujibu Jux, anaamini kustahilishi kuwania vipengele vya Video Bora, Wimbo Bora wa Bongo Fleva, Msanii Bora wa Bongo Fleva, Msanii Bora wa Kiume, Mtunzi Bora na Mtumbuizaji Bora, vipengele ambavyo vyote amevikosa.

Kolabo yao ya tatu, Ololufe Mi (2024) ambayo Jux kamwimbia mkewe Priscilla kutokea Nigeria, imefanya vizuri na tayari imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 21 ikiwa ni miezi saba tangu itokea.

Sasa kufuatia kufanya vizuri kwa kolabo hizo mbili na Diamond, kumekuza sana chapa ya Jux kimuziki kimataifa akishinda tuzo za Trace kama Msanii Bora wa Kiume Tanzania 2024, na Headies kama Msanii Bora Afrika Mashariki 2025.

Katika data za YouTube kwa mwezi uliopita, Jux alishika nafasi ya pili katika orodha ya wasanii wa Tanzania waliotazamwa zaidi YouTube ikiwa ni mara ya kwanza kushika nafasi hiyo.

Diamond ndiye namba moja akiwa ametazamwa zaidi ya mara milioni 30, Jux milioni 18.5, kisha Marioo (18.1), Harmonize (15.1), Jay Melody (13.08), Rayvanny (13.04), Zuchu (11.5), Alikiba (8.3), Mbosso (8) na D (Voice 6.1).

Hatua hiyo inakuja wiki chache baada ya Jux kuachia EP yake ya kwanza, A Day To Remember (2025) yenye nyimbo saba na kuwashirikisha wasanii wawili ambao ni Phyno kutokea Nigeria na D Voice kutokea WCB Wasafi.

Utambuka wimbo ‘God Design’ kutoka katika EP hiyo, ulishika namba moja katika chati ya iTunes Nigeria akiwa ni msanii wa pili wa Bongofleva kufanya hivyo baada ya Diamond kupitia wimbo wake, My Bay (2023) akimshirikusha Chike wa Nigeria pia.

Hivyo, mbali na sababu nyingine, lakini ukweli Jux anang’aa kimataifa kutokana na mchango wa Diamond katika kazi walizotoa pamoja na sasa ameanza kusogelea soko la kimataifa ambalo ni ndoto ya wanamuziki wengi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags