Watimkia ughaibuni na sanaa yao

Watimkia ughaibuni na sanaa yao

Peter Akaro

Watu kuhama nchi zao kwa kipindi fulani na kwenda kuishi ughaibuni sio jambo geni kwani ni utamaduni wa miaka mingi, utafutaji wa fursa za kimaisha, masomo na familia kunatajwa kuchochea hilo kwa kiwango fulani.

Katika tasnia ya sanaa Bongo tumeshuhudia baadhi ya wasanii kutoka kwenye muziki na filamu wakienda kuishi nje huku wakiendeleza sanaa yao na wengine wakiacha kabisa. Hawa ni baadhi yao.

1. Roma - Marekani

Tangu Novemba 2019 Roma yupo Marekani, mwanzoni alieleza kilichompeleka nchini humo ni mualiko maalum alioupata kutoka kwa jamii ya watu wanaozungumza Kiswahili wanaoishi Marekani maarufu kama SUSA (Swahili society USA).

Licha ya kuwa huko ameendelea kutoa nyimbo, miongoni mwa hizo ni Kaka Tuchati (2020), Watani wa Jadi (2020), Sifa (2021) na Hujambo Mwanangu (2021), zote zikiwa za kundi la Rostam. Pia kuna zake kinafsi kama Diaspora (2020), Nasikia Harufu (2024) nk.

Utakumbuka Roma alipata mafanikio zaidi kimuziki alipotoa wimbo wake, Mathematic (2012) ambao ulimuwezesha kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Hip Hop.

2. Ray C - Ufaransa

Mwimbaji huyo ni kipindi kirefu haishi nchini, kabla ya kwenda Ufaransa alikaa Kenya kwa muda huku akiendelea na shughuli zake za muziki kwa kiasi fulani baada ya kupata menejimenti nchini humo.

Ndani ya Ufaransa amekuwa na shughuli zake binafsi nje ya muziki, hata hivyo aliwahi kueleza kuwa amekuwa akitumbuiza (Kariyoki) kwenye kumbi mbalimbali za starehe kabla ya biashara hiyo kuathiriwa vibaya na mlipuko wa virusi vya Corona.

Ray C ambaye Februari 2023 alijaliwa mtoto akiwa Ufaransa, alianza kuvuma kimuziki chini ya Smooth Vibe baada ya kurudia wimbo wa Gwiji wa Taarab, Nasma Hamis, Mahaba ya Dhati kisha zikafuata nyimbo zake nyingine kama Upo Wapi na Na Wewe Milele.

3. Mr. Beneficial & Bwana Mjeshi - Marekani

Hawa ni wachekeshaji maarufu kutoka kundi la Timamu Comedy, ni takribani miaka mitano sasa wapo Marekani na Bosi wao, Timoth Conrad wakiendelea na shughuli zao za sanaa na mambo mengine binafsi.

Wakiwa nchini humo wameachia filamu, Nothing Else (2021) ambayo ni ya kwanza kwa wasanii kutokea Tanzania kuingia kwenye mitandao ya Amazon Prime na Vimeo ambapo walisaini mkataba wa miaka minne kufanya kazi pamoja.

Ikumbukwe Nothing Else ni filamu ya pili kwa waigizaji hao mara baada ya kuachia SEMA (2018) ambayo Ebitoke alikuwepo ndani yake kama muhusika mkuu, ni kabla ya kuja kuachana na kundi la Timamu Comedy ambalo ndilo lilimtoa kisanaa.

4. Vanessa Mdee - Marekani

Akiwa Marekani ndipo Vee Money alitangaza kuachana na muziki wa Bongofleva, anaishi huko na mchumba wake, Rotimi aliyemvisha pete ya uchumba mnamo Desemba 2020 na sasa tayari wana watoto wawili, Seven (2021) na Imani (2023).

Vanessa akiwa mdogo aliishi pia nchini humo kutokana na kazi ya baba yake mzazi, zaidi ya familia hajaweka wazi ni jambo gani hasa jingine anafanya huko, huku mchumba wake mwenye asili ya Nigeria akiendelea na muziki na filamu.

Hadi Vee anaacha muziki alikuwa ametoa albamu moja, Money Mondays (2018), ameshinda tuzo za TMA, AFRIMA na AFRIMMA, ameanzisha lebo, Mdee Music, huku akifanya mahojiano na Kelly Rowland, Rick Ross na Ludacris katika kazi yake ya awali.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags